GRUMETI FUND YATOA ELIMU YA KIJINSIA KWA WANAFUNZI ZAIDI YA 1000 SERENGETI

 

SHIRIKA la Grumeti Fund  kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imewaleta pamoja wanafunzi wa kike 688 na wakiume 671 kutoka katika shule za sekondari Issenye, Nagusi na Rigicha zilizopo wilayani Serengeti ili kujadili namna bora ya kujenga jamii yenye ushirikiano wa pamoja kati ya vijana wa kike na kiume na hatimae kujenga jamii yenye usawa miongoni mwa vijana wa jinsia zote.

Akizungumza katika kongamano lililofanyika kwa siku mbili katika shule ya sekondari Issenye na kuhusisha wanafunzi wa kike na kiume kutoka shule za sekondari Issenye, Nagusi na Rigicha, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel amewataka vijana hao kuyapa mambo ya msingi nafasi na kuacha kushughulika na mambo yasiyo ya msingi katika safari ya kutimiza ndoto zao ambapo amewataka kumtanguliza Mungu katika kila jambo kwani ndio msingi wa mafanikio.

"Tuachane na mambo yasiyofaa ili tuweze kuyapa nafasi mambo ya msingi kuweza kuchukua nafasi katika vichwa vyetu, tunakosea kushughulika na mambo yasiyo na maana na tukayaacha yale yenye msaada kwetu kwa kuiga baadhi ya vitu ambavyo sio utamaduni wetu kwa hali hii hatutafika popote labda Mungu aingilie kati, Niwatie moyo sasa kuwa bado hamjachelewa bado mnayonafasi ya kubadilika na kuwa vijana wenye kutegemewa na familia zenu kama mkimtanguliza Mungu na ndio maana sisi Grumeti Fund kwa kutambua umuhimu wenu tumekuja kuwatia moyo kuwa unaweza kuwa mtu yeyote endapo utajitambua na kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mungu katika kila jambo, tambueni kuwa mkisoma kwa bidii na kupata maarifa na ujuzi  ndivyo vitu vitakavyokuokoa katika dunia hii" ,alisema Bi. Frida
Aidha, Bi. Frida ametoa msisitizo kwa vijana hao kuwa mstari wa mbele katika kukataa na kupinga mila na desturi za kigeni zinazoenda kinyume na maadili na chukizo kwa Mungu kwa kuwa na msimamo na maamuzi kwani ndio msingi wa kutotumbukia katika vishawishi vya dunia  ya utandawazi.

Katika kongamano hilo shirika la Grumeti Fund imetoa Mipira na jezi za michezo  Kwa shule zote tatu zilizoshiriki kwa wanafunzi wa kiume na  kutoa msaada wa taulo za kike  zinazoweza kutumika  kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa wanafunzi wa kike 688 zenye thamani ya Shilingi 10,320,000/- katika shule za sekondari Issenye, Nagusi na Rigicha.

Naye mgeni rasmi  katika kongamano la wasichana Bi. Pelesia Manyama ambaye ni Katibu wa chama cha Walimu, amewataka wasichana kujitambua thamani yao sambamba na kuweka dira ya maisha yao mbele ili kuepuka changamoto za kimaisha huko baadae, huku akiwataka kumfanya Mungu kuwa mtatuzi wa changamoto zao na kuepuka ushawishi.

"Mfanye Mungu kuwa mtetezi wako katika kila jambo gumu lililokosa majibu, niwaambie kuwa ukimcha Mungu utaepuka mambo mengi mabaya, hata sisi tulivyo hivi ni kwasababu tuliwekeza katika kumcha Mungu na bado tunamtegemea yeye hadi sasa, bila Mungu dunia na tamaa zake zitakumeza. Ili kufanikiwa katika masomo yako jitahidi sana kuwa na hofu ya Mungu pamoja na kuwekeza katika masomo yenu" Jiepusheni na marafiki wabaya na mambo yasiyo na tija",alisema Bi. Pelesia Manyama.
Kwa upande wake  mkufunzi kutoka  chuo cha Afya Kisare Mwl. Restuda Murutta akitoa Elimu ya uzazi kwa wanafunzi wa kike amewaasa kuzingatia usafi wawapo katika siku za hedhi na  kuwataka kuzitumia taulo za kike zilizotolewa na Grumeti Fund kwa usahihi sambamba na kuepuka vishawishi vitakavyo waingiza katika kufanya mapenzi katika umri mdogo na mwisho kupelekea ndoa za utotoni.

“Usafi wakati wa hedhi ni muhimu sana kwani utaepuka magonjwa mbalimbali, lakini pia inasikitisha binti anaumri chini ya miaka 18 ameshaanza kujiingiza kwenye mahusiano ya ngono kitu ambacho sio salama, kabla ya kuingia kwenye mambo hayo kwanza jiulize je ni umri sahihi wa kuingia kwenye mambo hayo ukishapata jibu acha", alisema Bi. Restuda

Naye aliyekuwa Mgeni rasmi katika kongamano la wanafunzi wa kiume  anayehudumia idara ya vijana katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Emmanuel Samuel Sitta amewaasa vijana wa kiume kukujitambua kuwa wao ni wanaume na wameumbwa na Mwenyezi Mungu kama wanaume Kwa makusudi.
"Nataka niwaambie, ili tuweze kuwa salama kama watoto wa kiume lazima tujenge jamii yenye hofu ya Mungu ndani yake, siku hizi imezuka tabia ya wanaume kutamani kufanya mambo ya jinsia ya kike hii yote ni kutokana na vijana wengi kukosa hofu ya Mungu, Sasa tambueni kuwa wewe umeumbwa na Mungu kama mwanaume hivyo unatakiwa kufanya yale yaliyowekwa na Mungu ili yafanywe na wanaume na si vinginevyo " ,alisema Mchungaji Sitta.

Nao miongoni mwa wanafunzi wa kike na kiume waliopata mafunzo wameishukuru kampuni ya Grumeti Fund kwa namna wanavyowajali na kuwathamini vijana wa kike na kiume katika kujenga jamii bora yenye usawa na kuahidi kuyaweka katika vitendo mafunzo hayo na kusambaza elimu kwa wengine.

Kwa takribani miaka saba kampuni ya Grumeti Fund imekuwa ikitoa elimu ya kijinsia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za sekondari mbalimbali Wilayani Serengeti na Bunda ambapo tangu mwaka 2017 hadi awamu hii ya tatu  ya kongamano hili kwa Mwaka 2024  imefanikiwa kutoa elimu ya kijinsia kwa wasichana 12,085 na kutoa taulo 12,085  kwa kila binti anayeshiriki mafunzo hayo, huku ikifanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana zaidi ya 6,945 tangu mwaka 2021 hadi awamu hii  ya nne ya kongamano la Mwaka 2024 na kutoa zawadi za jezi na mipira  kwa kila shule iliyoshiriki kwenye kongamano.

 

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA