*Ni kupitia Mkutano wa Wiki ya Mafuta Afrika*
*Aeleza jinsi Sheria za Tanzania zinavyowiana na mazingira ya uwekezaji*
*Asema Tanzania ina miundombinu wezeshi ya usafirishaji bidhaa za mafuta na Gesi Asilia*
*Aeleza miradi inayotoa hakikisho la uwepo wa umeme wa kutosha*
*Asisitiza Nishati Safi ya Kupikia ni ajenda ya nchi*
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaanza zoezi la kunadi vitalu 24 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia mwezi Machi 2025 katika kipindi cha Kongamano na Maonesho ya Mafuta na Gesi Asilia Afrika Mashariki yatakayofanyika nchini.
Mhe. Judith Kapinga amesema hayo wakati akihutubia Kongamano la Wiki ya Mafuta Afrika linalofanyika nchini Afrika Kusini ambalo limehudhuriwa na washiriki kutoka nchi 70 duniani kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu mafuta na gesi asilia.
Kapinga amesema katika duru la tano la kunadi vitalu vya gesi asilia, Wizara ya Nishati imejipanga kuvitangaza vitalu vyote 24 ambapo visima 21 vipo Bahari ya Hindi na vingine vipo ziwa Tanganyika.
Ameeleza kuwa, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zilianza miaka ya 1950 ambapo hadi sasa kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa ni takriban futi za ujazo Trilioni 57.
Amesema gesi asilia inatumika kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, nishati katika magari, viwandani na majumbani huku lengo likiwa ni kuendana na ajenda ya kimataifa ya mabadiliko ya nishati pamoja na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, amesema hiyo ni ajenda ya nchi na kinara wake ni Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anashirikiana na wadau wengine kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafikiwa.
Kupitia mkutano huo, Mhe. Kapinga ameeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini kupitia Wizara ya Nishati pamoja na kuwaalika wawekezaji kuwekeza nchini.
Amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Kuhusu sekta ya umeme, Kapinga amebainisha miradi inayofanyika nchini kwa ajili ya kuimarisha gridi ya Taifa, ikiwemo mradi wa umeme Jua Kishapu, mradi wa Julius Nyerere utakaozalisha megawati 2,115 pamoja na miradi mingine ikiwemo ya upepo ili kuhakikisha gridi inaimarika.
Akizungumzia uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji nchini, Kapinga amesema Serikali imeshapitia Sheria ya Petroli na mkataba kifani wa uzalishaji na ugawanaji mapato kwa lengo la kuhakikisha masharti ya kiuchumi na kisheria yanakuwa na usawa kiushindani katika sekta ya mafuta kwenye ngazi ya kikanda na kimataifa.
Aidha, amewaeleza washiriki wa kongamano kuhusu mifumo ya kisheria yenye uwiano kwa kuzingatia mazingira ya uwekezaji.
Vilevile, Kapinga amewahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kutokana na uwepo wa miundombinu wezeshi ambayo inarahisisha usafirishaji wa bidhaa za mafuta na gesi asilia ikiwemo bomba la gesi asilia kutokea Mtwara hadi Dar es Salaam, mitambo mitatu ya kuchakata gesi asilia, bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki na bomba la mafuta kutoka Tanzania hadi Zambia.
Viongozi wengine waliohudhuria Kongamano hilo ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Kamishina wa Petroli na Gesi, Godluck Shirima; Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Y. Sefue Mwenyekiti wa Bodi ya PURA, Halfani Halfani, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA), Mha. Charles Sangweni pamoja na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na taasisi zake.
إرسال تعليق