SERIKALI KUSOMESHA WATAALAMU BINGWA NA WABOBEZI 300 KILA MWAKA


 Waziri wa Afya wa Tanzania Jenista Mhagama, amesema kuwa Wizara ya Afya imejiwekea lengo la kusomesha wataalamu bingwa na wabobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Serikali, unaojulikana kama ‘Samia Health Specialization Scholarship Program’.


Akiwasilisha taarifa hii ofisini kwake jijini Dodoma, Jumatatu Oktoba 21, 2024, Waziri Mhagama amesisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi, na kuvutia tiba utalii.

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga jumla ya shilingi bilioni 14 kugharamia mafunzo ya wataalamu wapya 544 katika mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi, pamoja na wataalamu wengine 47.

Fedha hizo ni ongezeko la shilingi bilioni 3.05, sawa na asilimia 28 zaidi ya bajeti ya mwaka uliopita wa fedha wa 2023/2024, ambao ulitenga shilingi bilioni 10.95. Waziri Mhagama amesema kuwa ongezeko hili ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba sekta ya afya inapata wataalamu wa kutosha wenye ujuzi wa hali ya juu.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, Wizara ilipokea jumla ya maombi 948 kutoka nchi nzima, ambapo waombaji wa kike walikuwa 353 (37%) na wa kiume 595 (63%). Kati ya hao, waombaji 771 walikidhi vigezo, na 544 walichaguliwa kufadhiliwa, sawa na asilimia 71 ya waombaji waliokidhi vigezo.” Ameeleza Waziri Mhagama akiongeza kuwa kati ya wataalamu waliochaguliwa, 95% wanasomea ndani ya nchi na 5% nje ya nchi.

Akiendelea kufafanua, Waziri Mhagama amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya wataalamu 829 ambao tayari wapo kwenye mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi wataendelea kufadhiliwa na Serikali. Ufadhili huo unajumuisha ada ya mafunzo, posho ya utafiti, na kwa wale wanaosoma nje ya nchi, watafadhiliwa posho ya kujikimu na nauli ya kwenda na kurudi.

Waziri Mhagama amehitimisha kwa kusema kuwa uwekezaji huu wa kimkakati ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya na utaongeza idadi ya wataalamu bingwa na wabobezi ambao watachangia katika kuboresha huduma za matibabu hapa nchini.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA