Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Thobias Makoba, akiongea katika ofisi za Sahara Media Group leo Oktoba 16, 2024, ambapo ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuhamasisha Watanzania kujitokeza kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Na Mwandishi wetu, Mwanza
Serikali imevihimiza vyombo vya habari nchini kuendelea kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Thobias Makoba, ametoa wito huo kwa vyombo vya habari leo jijini Mwanza baada ya kutembelea vyombo vya habari vya kampuni ya Sahara Media Group.
Bw. Makoba ameeleza kuwa moja ya wajibu wa vyombo vya habari ni kutoa elimu hasa nyakati muhimu kama kwenye chaguzi za ngazi mbali ukiwemo uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa ambapo kama vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuhamasisha wananchi kujiandikisha na baadae kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa viongozi mbalimbali.
“Serikali inavishukuru sana vyombo vya habari kwa kazi kubwa ya kuwahabarisha Watanzania na tunatoa wito viendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu zoezi muhimu la kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili Watanzania wote wenye sifa na vigezo wakajiandikishe”, amesisitiza Msemaji Mkuu wa Serikali.
Ameeleza kuwa mpaka sasa zoezi la uandikishaji linaendelea vyema na na kutoa wito kwa Watanzania wenye sifa na vigezo kutumia siku zilizobaki kwenda kujiandikisha ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia.
Aidha, pamoja na rai hiyo, katika mahojiano yake na RFA, Bw. Makoba amewashukuru wananchi wa Mkoa Geita na Mkoa wa Mwanza kwa mapokezi mazuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipofanya ziara katika mikoa hiyo kwa ajili ya shughuli za kitaifa.
Rais Samia alitembelea mkoa wa Geita kwa ajili ya kufunga Maonesho ya Teknolojia ya Madini na baadae alielekea mkoa wa Mwanza kushiriki Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Maadhimisho ya Kumbukizi ya miaka 25 tangu kufariki Baba wa Taifa , Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
إرسال تعليق