Mhandisi James Jumbe Wiswa, ambaye ni mdau mkubwa wa michezo na maendeleo ya jamii, ametimiza ahadi yake ya kusaidia timu 12 zinazoshiriki Ligi ya Taifa Ngazi ya Wilaya ya Shinyanga, maarufu kama "Dr. Samia – Jumbe Cup," kwa kutoa mchango mkubwa wa fedha kwa ajili ya masuala mbalimbali yanayohusu ligi hiyo.
Mchango wa Mhandisi Jumbe alioahidi na kutoa ni Shilingi Milioni 2.4 kwa ajili ya maji ya wachezaji wa timu 12 zinazoshiriki Ligi ya Wilaya, Shilingi 800,000/= kwa ajili ya waamuzi wa michezo, Shilingi 850,000/= kwa ajili ya vifaa vya michezo kwa waamuzi na Shilingi Milioni 3 kwa ajili ya timu tatu zinazoshiriki Ligi ya Mkoa ambapo Jumla ya mchango wa fedha zote, ikiwa ni pamoja na vifaa na fedha alizotoa kutimiza ahadi, inafika Shilingi 7,050,000/=.
Katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo iliyofanyika Novemba 2, 2024, katika Uwanja wa CCM Kambarage, ambapo Mhandisi Jumbe alikabidhi vifaa vya michezo kwa timu zote 12 zinazoshiriki mashindano hayo, huku akiahidi zawadi nono kwa washindi kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tano.
Katika uzinduzi huo, Mhandisi Jumbe alitangaza zawadi ya kipekee kwa timu zitakazoshinda mashindano hayo. Mshindi wa kwanza atapata ng'ombe, kilo 200 za mchele, kreti nne za soda pamoja na shilingi milioni tatu. Mshindi wa pili atapata shilingi Milioni mbili, ng'ombe, mchele kilo 200 na Kreti nne za soda, na wa tatu ataondoka na zawadi ya shilingi Milioni moja , ng'ombe, mchele kilo 200 na kreti 4 za soda huku washindi wa nafasi ya nne na ya tano wakipata mbuzi wawili, kilo 100 za mchele, na shilingi 200,000/= kila mmoja.
Mhandisi James Jumbe
Mbali na msaada kwa timu zinazoshiriki Ligi ya Taifa, Mhandisi Jumbe aliahidi pia kutoa msaada wa shilingi milioni moja kwa kila timu inayoshiriki Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni Katunda FC, Boko FC, na Mshikamano Shy FC zilizopo katika Wilaya ya Shinyanga. Pia, aliahidi kuwapatia waamuzi wa mashindano vifaa vya michezo, ikiwa ni pamoja na jezi, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ahadi ambayo ameitekeleza Novemba 5,2024 na Novemba 8,2024.
Ahadi zote hizo zimetekelezwa, na fedha hizo zimekabidhiwa kwa niaba ya Mhandisi Jumbe na Masuka Jumbe Novemba 5, 2024, katika Uwanja wa CCM Kambarage.
Zawadi hizi ni sehemu ya jitihada za Mhandisi Jumbe kutia moyo wachezaji na kuendeleza vipaji vya vijana wa Shinyanga.
“Wachezaji wa Shinyanga wanapaswa kuona kuwa michezo ni njia muhimu ya kufikia malengo yao maishani. Huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika mpira wa miguu wa Shinyanga, na nitatumia kila fursa kuhakikisha vipaji vya vijana wetu vinapata nafasi ya kung'ara,” alisema Mhandisi Jumbe wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo.
Mashindano ya Dr. Samia – Jumbe Cup ni mfano mzuri wa jinsi watu binafsi wanavyoweza kutumia rasilimali zao kuendeleza michezo na kutoa nafasi kwa vijana kufikia malengo yao.
Mashindano ya Dr. Samia – Jumbe Cup ni kipengele muhimu cha maendeleo ya michezo katika Shinyanga na Mhandisi Jumbe amedhihirisha kuwa kuwekeza katika michezo ni kuwekeza katika kizazi kijacho, kwani michezo hutoa fursa ya kukuza vipaji, kukuza nidhamu na kuhamasisha umoja katika jamii na kwa umoja wa wadau, Shinyanga itakuwa na nafasi kubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Mhandisi James Jumbe
Mhandisi Jumbe ameonyesha kwa vitendo namna ambavyo anaweza kusaidia vijana wa Shinyanga kufikia malengo yao kupitia michezo.
Msaada huu wa kifedha na vifaa vya michezo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha michezo katika mkoa wa Shinyanga.
Mashindano ya Dr. Samia – Jumbe Cup yamekuwa ni jukwaa muhimu la kuonyesha vipaji vya wachezaji wa Shinyanga na timu 12 zinazoshiriki mwaka huu ni: Lwambogo FC, Upongoji FC, Original FC, Upongoji Star, Qatar FC, Mwadui United, Kitangili United, Rangers FC, Magereza FC, Kambarage Market na Waha FC.
إرسال تعليق