-Kapinga ataja msamaha wa kodi asilimia 25 kwa injini za magari yanayotumia gesi asilia iliyotolewa 2023/2024.
-Aeleza Serikali ilivyojidhatiti kupeleka umeme kwenye maeneo yote nchini.
Na Mwàndishi Wetu
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema kupitia Bajeti Kuu Serikali ya mwaka 2023/24 Serikali ilitoa msamaha wa kodi ya ushuru wa forodha (customs duty) asilimia 25 kwa injini za magari yanayotumia gesi asilia yanapoingizwa nchini.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Novemba 06, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kupunguza baadhi ya kodi kwenye magari yanayotumia mfumo wa gesi ili Watanzania wengi waweze kuyaagiza.
"Tuaendelea na hatua mbalimbali za kuhamasisha sekta binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye viwanda vinavyo tengeneza vipuri vinavyotumika katika kufunga mfumo wa matumizi ya gesi asilia kwenye magari na mitambo hapa nchini", Amesema Mhe. Kapinga
Kuhusiana na usambazaji wa umeme Vijijini, Vitongojini na kwenye mitaa Mhe. Kapinga amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati imejidhatiti kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata huduma ya umeme.
Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Ester Matiko aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kubadili magari yanayotumia mfumo wa dizeli kwenda kwenye gesi, Mhe. Kapinga amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye vituo zaidi ili kuhakikisha pia na magari yanayotumia dizeli yanaanza kutumia mfumo wa gesi.
Ameongeza kuwa kutokana na utofauti uliopo kati ya magari yanayotumia petroli na dizeli ilikuwa ni rahisi kwa Serikali kuanza na magari ya petroli kabla ya yanayotumia dizeli.
Akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Mjini, Mhe. Ally Juma aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itapeleka Mradi wa umeme wa Vijijini kwenye Mitaa ya Tampori, Kwamtwara, Chemichemi, Chandimo, Dumi, Hachwi na Guruma - Kondoa, Mhe. Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na kazi ya utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme katika maeneo ya vijijini na vitongojini na vijiji vyote vya Jimbo la Kondoa Mjini vimefikishiwa umeme.
Ameongeza kuwa., Mitaa ya Tampori na Chemichemi itapatiwa umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 kwa kila Jimbo.
Mhe. Kapinga amesisitiza Serikali kupitia TANESCO na REA inaendelea kuratibu kazi za kusambaza umeme katika mitaa ya Kwamtwara, Chandimo, Dumi, Hachwi na Guruma kulingana na upatikanaji wa fedha.
Post a Comment