TANZANIA KUWA MWENYEJI MKUTANO WA KIKANDA KWA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI NA SADC UNAOHUSU MATUMIZI YA NISHATI

 


TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unaohusu masuala ya Matumizi Bora ya Nishati.

Mkutano huo utafanyika jijini Arusha kuanzia Desemba 4 mpaka Desemba 5 mwaka huu na umeandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa Kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Ubalozi wa Ireland.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema mkutano huo unatokana na programu ya pamoja yaTanzania, UNDP, EU na Ubalozi wa Ireland inayohusika na Matumizi Bora ya Nishati iliyoanza kutekelezwa mwaka 2022.

Akifafanua zaidi Mhandisi Luoga aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba katika mkutano huo mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Dotto Biteko na utahusisha wadau wa nishati takriban 400.

Amesema miongoni mwa wadau hao wamo mawaziri, wataalam na sekta binafsi na kuongezea wakati wa mkutano huo masuala yanayohusu matumizi bora ya nishati yatajadiliwa hasa kwa kuzingatia kwa sasa wamekuwa wakiwahimiza wananchi kutumia vifaa vinavyotumia umeme mdogo wenye gharama nafuu.

Akielezea zaidi pogramu ya Matumizi Bora ya Nishati, Mhandisi Luoga ameeleza ina umuhimu mkubwa nchini kwani inahusisha matumizi ya umeme kwa ufanisi na kwa ubora na lengo kubwa ni kupunguza upotevu wa umeme, kupunguza gharama za umeme na kulinda mazingira.

Hata hivyo wakati wadau wakitarajiwa kukutana, Mhandisi Luoga amesema Tanzania tayari imeshaandaa mkakati wa matumizi bora ya nishati wa miaka 10 (2024-2034), kumekuwa na ufadhili wa wanafunzi wa kike katika masuala ya nishati.

"Pia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeshaanza kuandaa viwango vya matumizi bora ya nishati kwenye vifaa mbalimbali kama majokofu, pia kuna vijana takriban 152 wamepata ufadhili kutokana na ubunifu katika matumizi bora ya nishati."

Ametumia nafasi hiyo kuwashauri Watanzania kutumia vifaa vyenye viwango vya ufanisi bora wa nishati ili kudhibiti upotevu wa umeme na kutumia gharama ndogo katika matumizi ya umeme huku akifafanua kwamba kwa sasa wamefanikiwa kudhibiti upotevu wa umeme kutoka asilimia 21 mpaka asilimia 14.

Ameongeza na mkakati uliopo ni kuendelea kudhibiti upotevu huo mpaka kufikia asilimia tisa."Kutokana na maboresho ya miundombinu ya umeme tunayoendelea kufanya tumefanikiwa kudhibiti upotevu wa umeme kwa asilimia 14 kutoka asilimia 21 iliyokuwepo mwaka 2018.

"Hata hivyo tunaendelea kutoa rai kwa wananchi nao kuendelea kudhibiti upotevu wa umeme kwa kuangalia mfumo wa umeme katika nyumba au majengo Yao sambamba na kutumia energy server ambayo inasaidia kuwa na matumizi madogo ya umeme,kwa mfano unaweza ukatumia taa Mwanga mkubwa lakini zinatumia umeme mdogo."

Kwa upande wake, Programu Meneja wa Miradi ya Nishati kutoka EU, Massimiliano Pedretti ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa programu hiyo ambayo imeonesha mafanikio makubwa na kueleza kuwa Umoja huo utaongeza muda wa utekelezaji wa programu hiyo nchini ambayo ilikuwa ikifikia ukomo mwaka huu wa 2024 lakini sasa itaisha mwaka 2025 pamoja na kutanua wigo wa kazi pamoja na ufadhili.

Kuhusu mkutano wa Desemba 4 mpaka Desemba 5 mwaka huu utakaohusisha wadau wa nishati,amesema wanatarajia mengi yatajadiliwa wakati wa mkutano lakini ni matamanio Yao kuona nchi hizo zinakuwa na malengo ya pamoja katika kutekeleza Mpango wa matumizi bora ya nishati.

Kwa upande wake Naibu Balozi wa Ireland nchini, Mags Gaynor amesema Ubalozi huo unafurahishwa na jinsi Tanzania inavyotekeleza Programu ya Matumizi Bora ya Nishati ikiwemo kuandaa mkakati utakaopelekea Tanzania kutekeleza kwa ufanisi zaidi programu husika.

Kuhusu Mkutano huo wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati, amesema ni hatua kubwa katika safari ya mabadiliko kuelekea kwenye matumizi bora ya nishati pamoja na kuwa njia ya kusukuma ajenda ya matumizi bora ya nishati.

Kwa upande wake Abbas Kitogo, Mtaalam wa Miradi kutoka UNDP, amesema Mkutano huo utakuwa ni sehemu ya kubadilisha ujuzi, uelewa na kuhakikisha kunakuwa na uelekeo mmoja katika matumizi bora ya nishati kwani kila mmoja akifanya juhudi matumizi ya nishati yanatupungua na kuelekezwa kwenye sehemu zenye uhitaji.

Amesema pia kupunguza matumizi ya nishati kutasaidia kupunguza gharama za nishati ambazo zinaweza kuelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.

"Katika jengo letu kupitia watalaam ambao wamepatikana katika programu zetu za kupunguza matumizi ya nishati wametuwezesha sasa tutumie nusu ya umeme tulikuwa tunatumia awali na hata gharama zimepungua."
                                                      Chanzo - Michuzi tv.








Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA