-Asisitiza ubora wa mafunzo na uongozi bora
Na Happiness Shayo- Kilimanjaro
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua rasmi Bodi ya Magavana ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori MWEKA huku akisisitiza chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo bora yanayokidhi mahitaji kulingana na vipaumbele vya taifa samba na kupiga vita vitendo vya rushwa, ubadhirifu, wizi, na unyanyasaji wa kijinsia.
Mhe. Chana ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 29,2024 wakati wa akizindua Bodi hiyo Mkoani Kilimanjaro ambapo ameielekeza Bodi hiyo kuweka mikakati ya kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Mimi pamoja na uongozi mzima wa Wizara tuna imani kubwa nanyi kuwa kwa kutumia weledi, ujuzi na uzoefu wenu mtakisaidia Chuo hiki ambacho kwa miaka mingi kimekuwa kiwanda kikubwa na muhimu cha kuzalisha wataalamu wa wanyamapori na utalii, si ndani ya Tanzania tu, bali duniani kote” amesema Mhe. Chana.
Mhe.Chana ameitaka pia Bodi hiyo kuandaa kozi mahsusi zitakazozingatia matumizi ya teknolojia kwenye usimamizi wa wanyamapori na utalii kwa lengo la kulinda na kuendeleza maeneo ya hifadhi kwa mifumo wa kidijitali hasa katika malipo ya kifuta jasho/machozi,udhibiti wa moto na ulinzi wa misitu.
Katika hatua nyingine Mhe.Chana ameielekeza Bodi hiyo kuimarisha miundombinu ya Chuo na vitendea kazi ili viendane na mahitaji ya elimu inayotolewa na kuimarisha tafiti na ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kujibu changamoto zinazokabili sekta za uhifadhi na utalii nchini na katika nchi za kikanda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori MWEKA, Prof. Yunus Daud Mgaya ameahidi yeye pamoja na timu yake kutekeleza majukumu kwa weledi, ufanisi na tija ili kufikia kwa matarajio na malengo ya Serikali.
“Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wangu tutahakikisha tunarejea, kuandaa mitaala pamoja kuongeza program za masomo zinazojibu changamoto mbalimbali katika sekta ya mazingira maliasili na utalii na pia kukifanya chuo kukubalika kama chuo mahiri cha kutoa mafunzo katika taaluma mbalimbali za uhifadhi, maliasili na utalii na hili tunalenga hasa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachana wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika( SADC)” amefafanua Prof. Mgaya.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mkuu wa Chuo hicho na Katibu wa Bodi, Prof. Jafari Ramadhani Kideghesho, Wajumbe wa Bodi, Uongozi wa Chuo na Viongozi wa Serikali ya wanafunzi.
إرسال تعليق