Waziri wa Afya, Jenista Mhagama katika Banda la Amret Tanzania akipokea maelezo kutoka kwa Dkt. Edwin Kilimba, Mkurugenzi wa mradi wa Afya Thabiti Amref Tanzania (wa kwanza kushoto) wakati wa maonesho ya shughuli zinazofanywa na wadau katika mapambano dhidi ya UKIMWI katika Viwanja vya Maji Maji mkoani Ruvuma ambako wiki ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani kitaifa yanafanyika.
****
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amelipongeza Shirika la Amref Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI, hasa kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa vidole (Biometric Fingerprint) kusaidia utoaji wa huduma bora za afya.
Mhagama ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake katika banda la Amref Tanzania kwenye Viwanja vya Maji Maji, Ruvuma, ambako maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya UKIMWI Duniani yanaendelea.
Akizungumza baada ya kupokea maelezo kutoka kwa Dk. Edwin Kilimba, Mkurugenzi wa Mradi wa Afya Thabiti wa Amref Tanzania,Waziri Mhagama amesisitiza umuhimu wa kuendelea na jitihada za pamoja katika kutokomeza UKIMWI.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho: "Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI".
Kwa ufadhili wa PEPFAR kupitia U.S CDC Tanzania, Amref Tanzania inatekeleza mradi wa Afya Thabiti kwa kushirikiana na mashirika ya CIHEB, Afya Plus, na TCDC.
Mradi huo unalenga kuboresha huduma za matibabu ya kufubaza VVU (ART) katika Mkoa wa Simiyu, Mara, na Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufanikisha malengo ya 95-95-95 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS).
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama katika Banda la Amref Tanzania akisalimiana na wafanyakazi, anayetoa utambulisho ni Dk. Edwin Kilimba, Mkurugenzi wa mradi wa Afya Thabiti Amref Tanzania.
Malengo ya 95-95-95 ni: Asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU kufahamu hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya watu waliogundulika na VVU kuanza matibabu na asilimia 95 ya watu wanaotumia matibabu kufikia kiwango cha kufubaza VVU.
Kwa zaidi ya miaka 30, Amref Tanzania imeendelea kuwa mshirika muhimu wa serikali na wadau wengine katika kuboresha mifumo ya afya nchini.
Dkt. Kilimba alibainisha kuwa mafanikio haya yanatokana na ushirikiano wa dhati na juhudi endelevu za wadau wote.
Wakati wa maadhimisho hayo, wananchi wanahimizwa kuchagua njia salama na sahihi za kujikinga na maambukizi mapya, huku wakihakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote.
إرسال تعليق