BENKI YA CRDB, COSTECH WASAINI MKATABA WA SHILINGI BILIONI 2.3 KUWEZESHA BIASHARA ZA VIJANA

  

Dar es Salaam. Tarehe 17 Aprili 2025: Katika kuimarisha ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana nchini, Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) wamesaini mkataba wa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kuziwezesha biashara changa za vijana.

Makubaliano hayo yaliyoshuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, ni sehemu ya Programu ya IMBEJU kupitia dirisha lake la IMBEJU BUNI yakilenga kuwasaidia vijana wabunifu nchini kupata elimu ya fedha na mitaji nafuu ya kukuza biashara zao.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Waziri Mkenda amesema: “Hii ni hatua ya kupongezwa inayochochea ukuaji wa uchumi wa ubunifu. Ushirikiano huu ni jibu la changamoto ya kukosekana kwa ufadhili kwa vijana wabunifu na ni kielelezo cha juhudi za serikali kujenga uchumi shindani wa viwanda wenye ubunifu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa ameeleza kuwa ushirikiano huu una akisi dhamira ya Benki ya CRDB kushiriki kujenga uchumi jumuishi.
“Tangu kuanzishwa kwa Programu ya IMBEJU Machi 2023, tulilenga kuwafikia vijana na wanawake waliopo pembezoni na kuwapa fursa za kifedha. Kupitia mkataba huu, tunatarajia kuwafikia vijana zaidi ya 1,000 na kuwapa mitaji wezeshi, mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha ili waweze kuendesha biashara endelevu kwa mfumo rasmi hivyo kuwa rahisi kwao kukua zaidi,” amesema Tully.

Katika kipindi hiki cha ushirikiano kati ya Benki ya CRDB na COSTECH, zaidi ya vijana 700 wabunifu wamefikiwa na kuwezeshwa kupitia dirisha la IMBEJU Buni ambalo ni mahsusi kwa ajili ya wabunifu wenye biashara changa kwa kuwapa mafunzo na mitaji wezeshi yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 5.
Katika utekelezaji wa mkataba uliosainiwa, kutakuwa na kamati ya pamoja ya usimamizi (Steering Committee) kati ya Benki ya CRDB, CRDB Bank Foundation na Tume ya Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kufanya tathmini, ufuatiliaji, na usimamizi madhubuti wa utekelezaji ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi wa kutosha kulifikia lengo lililowekwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amesema, “Tunaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kubuni na kustawi kibiashara. Ushirikiano huu na CRDB Bank Foundation ni muendelezo wa safari tuliyoianza mwaka 2023, na sasa tunaongeza msukumo zaidi kufanikisha ndoto za vijana wengi.”
Tangu kuanzishwa kwake, Programu ya IMBEJU imekuwa mfano wa kuigwa katika uwezeshaji jumuishi. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, programu hii imewezesha zaidi ya vijana na wanawake milioni moja na kutoa mitaji wezeshi zaidi ya TZS bilioni 20 katika sekta mbalimbali.

Kupitia madirisha yake ya IMBEJU BUNI, IMBEJU NG'ARA ambalo ni mahsusi kwa ajili ya wanawake, IMBEJU KILIMO kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo na IMBEJU UBIA kwa ajili ya kukuza ushirika wa kimkakati ili kutekeleza kwa ufanisi program mbalimbali za uwezeshaji kwa vijana na wanawake, CRDB Bank Foundation imefanikiwa kutoa uwezeshaji muhimu kwa ajili ya kukuza biashara changa za vijana na wanawake wajasiriamali kote nchini.








Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA