Na, Mwandishi Wetu - Fichuzi news blog- DODOMA
Takwimu zinaeleza kuwa watu 1,536,842 kati ya watu 1,690,948 wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) walikuwa wanatambua hali zao za maambukizi, Kadhalika, WAVIU 1,545,880 wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU ambapo watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni asilimia 96.4 huku kiwango cha maambukizi mapya ikiwa ni watu 60,000 kila mwaka ambapo vijana wanaopata VVU maambukizi ni takribani asilimia 34.3 ya maamukizi mapya na kwa kutambua hilo Serikali imewataka wananchi wote nchini kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu ambao bado ni tishio.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo Aprili 09, 2025 bungeni jijini Dodoma alipokuwa anawasilisha Mapendekezo ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mheshimiwa Majaliwa amesema "Katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kuratibu shughuli za UKIMWI kwa kutoa huduma endelevu na stahimilivu kwa WAVIU, kuimarisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ili uweze kufanikisha malengo ya nchi katika kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030, kuweka msukumo katika kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU." Amesema Mhe. Kassim Majaliwa Waziri Mkuu Bungeni Leo
Hata hivyo amewahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania hata mmoja atakayekosa huduma hizo.
"Sambamba na hayo, Serikali inatambua mabadiliko ya kisera kutoka kwa baadhi ya washirika wetu wa muda mrefu wa masuala ya UKIMWI, Kufuatia mabadiliko hayo, Serikali inachukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye eneo la utaoji huduma kwa WAVIU, hatua hizo zenye lengo la kuwezesha taifa letu kujitegemea zitaendelea kuchukuliwa pia katika maeneo mengine." Amesema Majaliwa
إرسال تعليق